Wednesday, October 31, 2012

Rais Kikwete kunguruma Arusha leo


  
“Kabla ya kuhutubia wakazi wa Arusha na vitongoji vyake, Rais Kikwete atazindua hospitali ya Ortumer na baadaye kuwa mgeni rasmi sherehe za uzinduzi rasmi wa Arusha kupanda hadhi kutoka manispaa kuwa jiji,”

Peter Saramba, Arusha
RAIS Jakaya Kikwete leo atahutubia mkutano wake wa kwanza wa hadhara jijini Arusha tangu kumalizika kwa uchaguzi Mkuu mwaka 2010, ulioshuhudia iliyokuwa ngome ya CCM, ikiangukia mikononi mwa Chadema.
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, atahutubia mkutano huo katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid, zikiwa ni siku nne tangu CCM kinyang’anywe kiti cha Udiwani Kata ya Daraja II, kilichonyakuliwa na Chadema.
Daraja II ni kati ya kata 29 zilizofanya uchaguzi mdogo Jumapili iliyopita, huku CCM ikifanikiwa kutetea kata zake 24 na kushuhudia tatu zikiangukia mikononi mwa Chadema iliyoshinda tano.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo alisema licha ya Rais Kikwete kuhutubia mkutano wa hadhara, atazindua miradi ya miundombinu na elimu katika Jiji la Arusha na Wilaya ya Monduli.
“Kabla ya kuhutubia wakazi wa Arusha na vitongoji vyake, Rais Kikwete atazindua hospitali ya Ortumer na baadaye kuwa mgeni rasmi sherehe za uzinduzi rasmi wa Arusha kupanda hadhi kutoka manispaa kuwa jiji,” alisema Mulongo.
Alisema Novemba 2, Rais Kikwete atakizindua rasmi Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo eneo la Tengeru wilayani Arumeru, baadaye atatembelea kiwanda cha A to Z kinachotengeneza vyandarua vyenye viuwatilifu vya kuua mbu.
Pia, ratiba hiyo inaonyesha Novemba 3, atatembelea Wilaya ya Monduli ambako atazindua Sule ya Msingi Sokoine kabla ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa barabara ya Arusha Minjingu.

No comments:

Post a Comment