Wednesday, October 31, 2012

Dk Magufuli ‘amwakia’ mkandarasi kwa uzembe


”Ni ukweli usiopingika kandarasi hafanyi kazi vizuri na nilikuomba uje uweke jiwe la msingi ili utakapoondoka, mimi, mkandarasi na mtaalamu mshauri ndipo tutakapokomeshana.”


WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amegeuka mbogo na kuipa Kampuni ya Atlantic Market Ltd siku 60 kumpa mpango jinsi itakavyokamilisha ujenzi wa barabara ya Kwasadala- Masama.
Dk Magufuli aliiagiza bodi ya wakandarasi nchini (CRB) kuichukulia hatua kampuni hiyo iwapo ndani ya siku hizo 60, itakuwa haijawasilisha mpango wa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ya kilomita 12.5.
Waziri Magufuli alikunjua makucha yake jana katika Kijiji cha Roo Masama Mashariki, wilayani Hai muda mfupi kabla ya Rais Jakaya Kikwete hajaweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh5.4 bilioni ulianza Mei 2010 na ulitakiwa uwe umekamilika na kukabidhiwa Mei mwaka jana.
Dk Magufuli alishukuru kwa sababu wakati wa utambulisho wa viongozi mbalimbali, alisikia alikuwapo Mkurugenzi mwendeshaji wa kampuni hiyo, Gabriel Mrema.
“Kwa taarifa tulizonazo ni kwamba mkandarasi ameshalipwa Sh1.6 bilioni na ameshatengeneza certificate (vyeti) saba na zote amelipwa, kwa hiyo haidai serikali kwa kazi aliyofanya,”alisema Dk Magufuli na kuongeza:
”Ni ukweli usiopingika kandarasi hafanyi kazi vizuri na nilikuomba uje uweke jiwe la msingi ili utakapoondoka, mimi, mkandarasi na mtaalamu mshauri ndipo tutakapokomeshana.”
Huku akishangiliwa na wananchi, Dk Magufuli alisema yeye hayupo tayari kufukuzwa kazi kwa sababu ya kilomita 12.5, hivyo anataka wahusika wawe wametangulia kufukuzwa.
Waziri Magufuli alisema baada ya Rais kuondoka eneo hilo, bodi ya wakandarasi na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), wakae na mkandarasi kujua watakavyoshughulika naye.
“Nakupa siku 60 uje na mpango wa kukamilisha barabara hii, usipofanya hivyo bodi ya makandarasi ianze kukushughulikia ikiwezekana ufutwe kabisa ukandarasi ili ukavue samaki,” alisema.
Alisema haiwezekani mkataba unasainiwa, mkandarasi anafanya kazi hovyohovyo kwa kutengeneza kilomita nne za lami kwa miaka mwili, huku akihoji kama angepewa kilomita 100 ingekuwaje.
Dk Magufuli alisema huo ni mfano wa makandarasi wazalendo ambao hivi karibuni walilalamika mbele ya Rais Kikwete kuwa, wananyimwa kazi na serikali na kupendelea kampuni za nje.
“Kwenye majukwaa wanalalamika kwamba makandarasi wazalendo hawapewi kazi, tena wakipewa bado kazi wanaiharibu… tukibembelezana hatutafika kama ni viboko tutandikane tu,” alifoka Dk Magufuli.
Alitumia fursa hiyo kumweleza Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe aliyekuwa ameketi jukwaa kuu kuwa, angalau sasa amefahamu mkandarasi ni tatizo katika kukamilisha barabara hiyo kwa wakati.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alisema ujenzi wa barabara hiyo aliamua yeye ijengwe kwa sababu katika wilaya nzima ya Hai, eneo la Masama ndilo pekee ambalo halikuwa na barabara ya lami.
“Kazi imeanza, lakini kwa bahati mbaya imechelewa sana sitaki kuingia kwenye sababu za kuchelewa, waziri amezieleza vizuri na kwamba alipoanza ziara aliarifiwa hakuna kinachoendelea,” alisema.
Rais Kikwete alisema licha ya kudokezwa hivyo, aliamua lazima aweke jiwe la msingi na anamini dosari zilizojitokeza zitamalizwa na ujenzi uanze kwa kasi kama ilivyotarajiwa.

No comments:

Post a Comment