Wednesday, October 31, 2012

Dk Magufuli ‘amwakia’ mkandarasi kwa uzembe


”Ni ukweli usiopingika kandarasi hafanyi kazi vizuri na nilikuomba uje uweke jiwe la msingi ili utakapoondoka, mimi, mkandarasi na mtaalamu mshauri ndipo tutakapokomeshana.”


WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amegeuka mbogo na kuipa Kampuni ya Atlantic Market Ltd siku 60 kumpa mpango jinsi itakavyokamilisha ujenzi wa barabara ya Kwasadala- Masama.
Dk Magufuli aliiagiza bodi ya wakandarasi nchini (CRB) kuichukulia hatua kampuni hiyo iwapo ndani ya siku hizo 60, itakuwa haijawasilisha mpango wa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ya kilomita 12.5.
Waziri Magufuli alikunjua makucha yake jana katika Kijiji cha Roo Masama Mashariki, wilayani Hai muda mfupi kabla ya Rais Jakaya Kikwete hajaweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh5.4 bilioni ulianza Mei 2010 na ulitakiwa uwe umekamilika na kukabidhiwa Mei mwaka jana.
Dk Magufuli alishukuru kwa sababu wakati wa utambulisho wa viongozi mbalimbali, alisikia alikuwapo Mkurugenzi mwendeshaji wa kampuni hiyo, Gabriel Mrema.
“Kwa taarifa tulizonazo ni kwamba mkandarasi ameshalipwa Sh1.6 bilioni na ameshatengeneza certificate (vyeti) saba na zote amelipwa, kwa hiyo haidai serikali kwa kazi aliyofanya,”alisema Dk Magufuli na kuongeza:
”Ni ukweli usiopingika kandarasi hafanyi kazi vizuri na nilikuomba uje uweke jiwe la msingi ili utakapoondoka, mimi, mkandarasi na mtaalamu mshauri ndipo tutakapokomeshana.”
Huku akishangiliwa na wananchi, Dk Magufuli alisema yeye hayupo tayari kufukuzwa kazi kwa sababu ya kilomita 12.5, hivyo anataka wahusika wawe wametangulia kufukuzwa.
Waziri Magufuli alisema baada ya Rais kuondoka eneo hilo, bodi ya wakandarasi na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), wakae na mkandarasi kujua watakavyoshughulika naye.
“Nakupa siku 60 uje na mpango wa kukamilisha barabara hii, usipofanya hivyo bodi ya makandarasi ianze kukushughulikia ikiwezekana ufutwe kabisa ukandarasi ili ukavue samaki,” alisema.
Alisema haiwezekani mkataba unasainiwa, mkandarasi anafanya kazi hovyohovyo kwa kutengeneza kilomita nne za lami kwa miaka mwili, huku akihoji kama angepewa kilomita 100 ingekuwaje.
Dk Magufuli alisema huo ni mfano wa makandarasi wazalendo ambao hivi karibuni walilalamika mbele ya Rais Kikwete kuwa, wananyimwa kazi na serikali na kupendelea kampuni za nje.
“Kwenye majukwaa wanalalamika kwamba makandarasi wazalendo hawapewi kazi, tena wakipewa bado kazi wanaiharibu… tukibembelezana hatutafika kama ni viboko tutandikane tu,” alifoka Dk Magufuli.
Alitumia fursa hiyo kumweleza Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe aliyekuwa ameketi jukwaa kuu kuwa, angalau sasa amefahamu mkandarasi ni tatizo katika kukamilisha barabara hiyo kwa wakati.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alisema ujenzi wa barabara hiyo aliamua yeye ijengwe kwa sababu katika wilaya nzima ya Hai, eneo la Masama ndilo pekee ambalo halikuwa na barabara ya lami.
“Kazi imeanza, lakini kwa bahati mbaya imechelewa sana sitaki kuingia kwenye sababu za kuchelewa, waziri amezieleza vizuri na kwamba alipoanza ziara aliarifiwa hakuna kinachoendelea,” alisema.
Rais Kikwete alisema licha ya kudokezwa hivyo, aliamua lazima aweke jiwe la msingi na anamini dosari zilizojitokeza zitamalizwa na ujenzi uanze kwa kasi kama ilivyotarajiwa.

Ruksa wafanyakazi kupata mafao ya kutoka mifuko ya jamii


“Mamlaka ya Usimamazi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), inapenda kuufahamisha umma kufutwa kwa tangazo lililotolewa na mamlaka Agosti 2012 kwenye vyombo mbalimbali vya habari lililohusu kusitishwa kwa fao la kujitoa,” ilisema sehemu ya taarifa ya SSRA.

SERIKALI jana iliwasilisha tamko bungeni kurejesha kwa fao la kujitoa katika mifuko ya jamii, ambalo liliondolewa na Mamlaka ya Kusimamia na Kudhibiti Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Agosti mwaka huu.
Akiwasilisha tamko hilo bungeni jana, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka alisema kwa kuzingatia mchakato ulioanza wa kuangalia upya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii, SSRA imeliondoa agizo la kuzuia mifuko kutoa fao la kujitoa.

Alisema kufuatia hatua hiyo , mifuko yote itaendelea kutoa fao hilo kama ilivyokuwa kabla ya zuio hilo na kwa vigezo vilevile kwa wanachama wanaostahili kupata fao hilo.

Waziri huyo alisema Serikali inaandaa muswada wa sheria wa kufanyia marekebisho sheria ya mifuko ya jamii sambamba na kuondoa katika muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali sehemu inayohusu fao la kujitoa.

Alisema kabla ya kuandaa muswada huo, Serikali itafanya majadiliano na wadau wote wakiwamo wabunge, vyama vya wafanyakazi, waajiri na wananchi.

Juzi SSRA ilitoa taarifa ya kufuta tamko lake la kuzuia fao la kujitoa kwa wanachama wa mifuko ya jamii nchini.

“Mamlaka ya Usimamazi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), inapenda kuufahamisha umma kufutwa kwa tangazo lililotolewa na mamlaka Agosti 2012 kwenye vyombo mbalimbali vya habari lililohusu kusitishwa kwa fao la kujitoa,” ilisema sehemu ya taarifa ya SSRA.

Pamoja na maelezo hayo, taarifa hiyo pia ilieleza kuwa uamuzi huo unaendana sambamba na hatua za Serikali za kuendelea na utekelezaji wa azimio la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao cha nane kilichoazimia pamoja na mambo mengine kuirejesha sheria ya hifadhi ya jamii.

Mhando atimuliwa rasmi Tanesco

Habari zilizopatikana juzi usiku na kuthibitishwa na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na wale wa Tanesco zinasema, Mhando alikabidhiwa rasmi barua ya kuachishwa kazi juzi.

HATIMAYE Serikali imemngíoa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuanzia juzi jioni.

Uamuzi wa kumwachisha kazi Mhando ulifikiwa katika kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo, ambacho kinadaiwa kwamba kilikuwa na mvutano mkali kabla ya kufikia makubaliano.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na bodi hiyo, Mhando ameachishwa kazi baada ya uchunguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kubainisha kwamba alikiuka taratibu za shirika hilo na kujihusisha na matumizi mabaya ya madaraka.

Taarifa hiyo pia ilisema kwamba Mhando ambaye awali, alisimamishwa kazi Julai 16, mwaka huu pamoja na maofisa wengine wa shirika hilo kutokana na tuhuma hizo baada ya kutiwa hatiani, Bodi hiyo ya Tanesco iliunda jopo la watu watatu kusikiliza utetezi wake kabla ya kuchukua hatua ambalo nalo pia lilimtia hatiani.
Bodi hiyo ilikutana Oktoba 29, mwaka huu na kujiridhisha kuwa Mhando alitenda makosa yanayohusiana na kuingia kwenye mikataba yenye mgongano wa kimasilahi kinyume na taratibu za shirika hivyo kufikia uamuzi wa kumwachisha kazi.

Habari zilizopatikana juzi usiku na kuthibitishwa na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na wale wa Tanesco zinasema, Mhando alikabidhiwa rasmi barua ya kuachishwa kazi juzi.

ìKilichomponza Mhando ni ule mkataba alioingia na mke wake wa Sh800 milioni wa kusambaza vifaa vya ofisini, hilo ndilo lilimponza na kwenye ripoti ya CAG wameweka wazi kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za zabuni,î kilisema chanzo kingine.

Mbali na Mhando, bodi hiyo pia iliwasimamisha kazi wafanyakazi wengine watatu ambao ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi Ununuzi, Harun Mattambo.

Hata hivyo, siku chache baada ya Mhando kusimamishwa kazi liliibuka kundi la watu wakiwamo baadhi ya wabunge, ambao walikuwa wakimtetea kwa madai kwamba alikuwa ameonewa.

Kundi hilo lilikwenda mbali zaidi na kutaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakimu Maswi wawajibishwe kwa uonevu huo.

Kadhalika, Profesa Muhongo na Maswi walidaiwa kwamba walimlazimisha Mhando kukiuka Sheria ya Ununuzi wa Umma katika mchakato wa kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme wa dharura.

Katika vita hiyo, zilizuka tuhuma kutoka kila upande, mvutano ambao baadaye ulizaa tuhuma kwamba baadhi ya wabunge walihongwa ili kukwamisha bajeti ya wizara hiyo.†

Tuhuma hizo zilisababisha Spika wa Bunge, Anne Makinda kuivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, kisha kuunda kamati ndogo ya kuchunguza tuhuma hizo za rushwa dhidi ya wabunge.

‘Ijumaa iwe siku ya mapumziko’

“Mbunge wa chama cha upinzani anatoa mchango wake anaambiwa kaa chini hata kama ana mchango mzuri kiasi gani… Spika akiwa kwenye chama fulani inaleta mpasuko”alisema.
Pia alitaka Katiba Mpya iweke kifungu kitakachoilazimisha Tume ya Uchaguzi (NEC),

MKAZI wa Kijiji cha Kikwe wilayani Siha, Halima Munisi ametaka katiba ijayo iitambue siku ya Ijumaa kuwa ni siku ya mapumziko kama zilivyo siku za Jumamosi na Jumapili.
Munisi alitoa pendekezo hilo juzi wakati akitoa maoni yake mbele ya kamati ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Profesa Mwesiga Baregu.
Kwa mujibu wa mwananchi huyo, Ijumaa kutokuwa ni siku ya mapumziko hasa kwa kuwa ndio siku ya kumuabudu Mola kwa Waislam si sahihi na kutaka siku hiyo iwe ya mapumziko.
Mkazi wa Kitongoji cha Nasai, Stanslaus Mallya alitaka katiba ijayo iweke kifungu ili Mawaziri watakaoteuliwa katika Baraza la Mawaziri wasiwe wabunge wa kuchaguliwa wala kuteuliwa.
Mallya alisema kitendo cha Mawaziri kushika kofia mbili ya Uwaziri na Ubunge, kinawafanya wasitekeleze majukumu yao ipasavyo hasa pale inapofikia mahali pa kuibana Serikali.
Kwa upande wake mkazi wa Ndoroso, Solomon Mmari alitaka Spika wa Bunge asiwe Mbunge na wala kuwa mfuasi wa chama chochote cha siasa ili aweze kutenda wajibu wake kwa haki.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Radegunda Nyabu, mkazi wa Magadini Bomang’ombe ambaye alisema endapo Spika anatokana na chama cha siasa, kuna kila sababu ya kutoa upendeleo.
“Mbunge wa chama cha upinzani anatoa mchango wake anaambiwa kaa chini hata kama ana mchango mzuri kiasi gani… Spika akiwa kwenye chama fulani inaleta mpasuko”alisema.
Pia alitaka Katiba Mpya iweke kifungu kitakachoilazimisha Tume ya Uchaguzi (NEC), kutopanga siku ya uchaguzi kwa siku zile ambazo zinatumika kumwabudu Mungu.
Kwa mujibu wa Nyabu, siku hizo ni Ijumaa kwa waumini wa Kiislam na Jumamosi na Jumapili kwa waumini wa Kikristo ili kila mmoja aweze kumwabudu na kumtukuza mola wake.

Rais Kikwete kunguruma Arusha leo


  
“Kabla ya kuhutubia wakazi wa Arusha na vitongoji vyake, Rais Kikwete atazindua hospitali ya Ortumer na baadaye kuwa mgeni rasmi sherehe za uzinduzi rasmi wa Arusha kupanda hadhi kutoka manispaa kuwa jiji,”

Peter Saramba, Arusha
RAIS Jakaya Kikwete leo atahutubia mkutano wake wa kwanza wa hadhara jijini Arusha tangu kumalizika kwa uchaguzi Mkuu mwaka 2010, ulioshuhudia iliyokuwa ngome ya CCM, ikiangukia mikononi mwa Chadema.
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, atahutubia mkutano huo katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid, zikiwa ni siku nne tangu CCM kinyang’anywe kiti cha Udiwani Kata ya Daraja II, kilichonyakuliwa na Chadema.
Daraja II ni kati ya kata 29 zilizofanya uchaguzi mdogo Jumapili iliyopita, huku CCM ikifanikiwa kutetea kata zake 24 na kushuhudia tatu zikiangukia mikononi mwa Chadema iliyoshinda tano.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo alisema licha ya Rais Kikwete kuhutubia mkutano wa hadhara, atazindua miradi ya miundombinu na elimu katika Jiji la Arusha na Wilaya ya Monduli.
“Kabla ya kuhutubia wakazi wa Arusha na vitongoji vyake, Rais Kikwete atazindua hospitali ya Ortumer na baadaye kuwa mgeni rasmi sherehe za uzinduzi rasmi wa Arusha kupanda hadhi kutoka manispaa kuwa jiji,” alisema Mulongo.
Alisema Novemba 2, Rais Kikwete atakizindua rasmi Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo eneo la Tengeru wilayani Arumeru, baadaye atatembelea kiwanda cha A to Z kinachotengeneza vyandarua vyenye viuwatilifu vya kuua mbu.
Pia, ratiba hiyo inaonyesha Novemba 3, atatembelea Wilaya ya Monduli ambako atazindua Sule ya Msingi Sokoine kabla ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa barabara ya Arusha Minjingu.

Mwenyekiti wa Bunge matatani kwa rushwa

 
NI AZZAN ZUNGU NA MAKADA WENGINE WA CCM, WAKAMATWA NA TAKUKURU, BULEMBO AELEKEA KUSHINDA

Waandishi Wetu, Dodoma
MMOJA wa Wenyeviti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu pamoja na makada wengine wa CCM, juzi usiku walikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Dodoma kwa tuhuma za rushwa.

Habari zilizopatikana mjini hapa juzi usiku zinasema, Zungu alikamatwa saa 4.30 katika moja ya vituo vya mafuta akidaiwa kujaribu kutoa rushwa ya Sh100,000 kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmari, jana alikiri kuwakamata baadhi ya watu wakijihusisha na vitendo vya rushwa akiwamo Zungu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mmari alidai kuwa vijana wake walimtia nguvuni Zungu juzi saa tatu usiku katika Hoteli ya Golden Crown akiwa na wapambe wake wakiendelea kugawa fedha kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wazazi.
Alisema taarifa za Zungu kudaiwa kugawa fedha hizo walizipata juzi mchana na kuanza kufuatilia nyendo zake ambazo zilionyesha kuwa na dalili zote za rushwa.
“Tuliweka mitego yetu kila mahali ndipo tukabahatika kukutana naye katika eneo la hoteli hiyo akiwa na magari mawili, moja ikiwa ni teksi ya kawaida na nyingine ikiwa ni Prado ambayo ndiyo ilisadikiwa kubeba pesa,” alisema Mmari.
Kamanda huyo alidai kuwa kiasi cha fedha kilichokuwa kikitolewa na Zungu kilikuwa Sh100,000 kwa kila mjumbe ili kumshawishi ampigie kura.
Hata hivyo, alisema hawakuweza kumkamata moja kwa moja akitoa na hata fedha hizo hawakuzikamata kwani maofisa wa Takukuru walizingira gari dogo wakati fedha hizo zinasadikiwa zilikuwa katika Prado ambalo baada ya vurugu hizo lilitokomea kusikojulikana.
Akizungumzia madai hayo Zungu alisema: “Kwanza niseme kuwa si kweli kwamba nimekamatwa nikitoa rushwa, nilikuwa katika kituo kimoja cha mafuta wakaja watu ambao walisema wana shaka na gari langu.”
Aliendelea: “Samahani, halikuwa gari langu, bali ilikuwa ni teksi, mimi nikawaruhusu, wakaingia wakafanya ukaguzi na waliporidhika wakaniachia nikaondoka.”

Taarifa za awali

Zungu alikuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia Wazazi katika uchaguzi uliofanyika jana mjini Dodoma.
Habari zilizopatikana mapema jana zilisema baada ya kukamatwa, Zungu alipelekwa Ofisi ya Takukuru Mkoa wa Dodoma ambako alihojiwa hadi saa nane usiku alipoachiwa baada ya kuwekewa dhamana na Mbunge wa Bukene (CCM), Selemani Zedi.
Habari hizo zinaeleza kuwa baada ya kukamatwa, gari alilokuwamo lilifanyiwa upekuzi kabla ya kupelekwa Ofisi za Takukuru, pamoja na makada wengine wa CCM ambao walikamatwa kwa tuhuma hizohizo.
Kamanda Mmari pia alithibitisha kukamatwa kwa makada wengine watano ambao aliwataja kuwa ni Yahaya Danga, Busuro Pazi na Frank Mang’ati ambao alidai kwamba walikuwa wakimsaidia Zungu katika mpango wake huo.
Mbali na watu hao, Takukuru ilimtia mbaroni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mbeya, Fatuma Kasenga ambaye anadaiwa kukamatwa akitoa rushwa ya chakula kwa wajumbe.
Alisema alikamatwa katika Hoteli ya Kitoli, Barabara ya Iringa saa tisa usiku.
Alisema kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja waliachiwa kwa dhamana na kwamba uchunguzi unaendelea.
Katika hatua nyingine, Mmari alisema kuwa taarifa walizokuwa nazo ni kuwa mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo alikuwa akitoa rushwa zaidi.
“Tatizo ni kwamba wanazungumza lakini hawatoi ushirikiano, maana kama wangetoa ushirikiano tungeweza kuwakamata kwa urahisi,” alisema Mmari.

Bunge hawajui

Akizungumzia kukamatwa kwa mbunge huyo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema Ofisi ya Bunge haikuwa na taarifa zozote kuhusu kukamatwa kwa mbunge huyo.
“Ndugu yangu, ndiyo nasikia kutoka kwako, sisi hatuna taarifa hiyo. Ni vigumu kuzungumzia jambo ambalo sijalisikia. Hata hivyo, nakushukuru sana kwa taarifa,” alisema Joel.

Rushwa CCM

Chaguzi za jumuiya za CCM zimekuwa zikilalamikiwa kugubikwa kwa vitendo vya rushwa na hata juzi baadhi ya wajumbe wa mkutano wa wazazi walilalamikia kuwapo kwa fedha nyingi kwenye uchaguzi huo.
Chaguzi nyingine zilizolalamikiwa kwa rushwa ni zile za Jumuiya ya Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake (UWT).
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wajumbe wa jumuiya hizo mbili kwa nyakati tofauti, alisema vitendo vya rushwa vinavyokithiri katika chaguzi za chama hicho, vinatishia uhai wake na kuwataka wanaCCM kubadilika.
Akifungua mkutano wa Jumuiya ya Wazazi jana, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal pia alizungumzia rushwa: “Hakuna sababu ya kumchagua kiongozi kwa kuwa tu amekupa kitu kidogo! Hakuna sababu ya mgombea kuamini kuwa ukitoa hongo na rushwa ndiyo utachaguliwa.
“Muda wa kampeni umekwisha na sasa mmebakiza saa chache mpigiwe kura. Sitegemei kuwa mtawapa tena nafasi wapambe wenu kujihusisha na vitendo vya rushwa ndani ya ukumbi wa mkutano.”
Mmoja wa wajumbe alimwambia mwandishi wetu juzi usiku kwamba rushwa iliyokuwa ikitolewa ni Sh100,000 kwa kila mjumbe, lakini fedha hizo zilikuwa zikitolewa kwa awamu, ya kwanza walipewa Sh70,000, wakati kiasi kilichobaki cha Sh30,000 walitarajiwa kupewa jana.

Nje ya ukumbi

Eneo linalozunguka Ukumbi wa Chuo cha Mipango ulikofanyika uchaguzi huo, jana lilihanikizwa na nyimbo za hamasa kuanzia saa 1.30 asubuhi zikitoka kwa wapambe wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.
Wapambe hao walikuwa wakiimba na kuzunguka nje ya uzio uliozunguka ukumbi huo, huku wakiwa wamevalia fulana zenye picha za wagombea wanaowaunga mkono na kubeba mabango yenye picha za wagombea hao.
Msafara wa mgombea wa uenyekiti, John Barongo ulioongozwa na pikipiki, magari madogo kwa makubwa na basi lililokuwa na wafuasi wake, uliwasili na kulakiwa na kundi la vijana waliokuwa wakimuunga mkono. Katika msafara huo, alikuwapo kada mkongwe wa CCM, Mzee Job Lusinde.
Baadaye, takriban dakika saba hivi, uliwasili msafara wa mgombea mwingine wa kiti hicho, Martha Mlata na wapambe wake na baadaye msafara wa Bulembo, hali iliyosababisha eneo hilo la nje ya uzio kushindwa kukalika kutokana na pilikapilka za kampeni za dakika za mwisho.
Shamrashamra hizo zilikoma baada ya kuwasili kwa Dk Bilal ambaye alifungua mkutano huo, kisha kukabidhi kazi ya kuuendesha kwa wasimamizi wa uchaguzi ambao ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Zakia Meghji.
Habari tulizozipata wakati tukienda mitamboni zinasema, Bulembo alikuwa akielekea kushinda nafasi ya uenyekiti akiwaacha mbali wenzake Mlata na Barongo.
Katika nafasi ya makamu mwenyekiti, uchaguzi huo ulitarajiwa kurudiwa baada ya wagombea wote kutofikisha nusu ya kura.